KINYANG'ANYIRO cha kuwania Ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini jana kilianza kwa mbwembwe baada ya wanachama watano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza kuwania ubunge katika Jimbo hilo.
Wanasheria wawili wa kujitegemea wa Jijini Arusha, Edmund Ngemela na Victor Njau ndio waliofungua pazia la kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kwa wana CCM wa Arusha Mjini kutaka kuteuliwa kuwania kiti hicho.
Njau ndiye mwana CCM aliyekwenda kuchukua fomu akiwa na msururu wa wapambe wa chama hicho, huku wakiimba nyimbo nyingi za kuwataka wanachama wa CCM kumuunga mkono mgombea huyo, ambaye wanadai ana sifa zote za kulikomboa jimbo hilo ambalo liko Chadema.
Wengine waliochukua fomu lakini hawakuwa na shangwe na mbwembwe nyingi ni Mahamudu Omari, Mosses Mwizarubi na Swalehe Kiluvia, ambao waliingia kuchukua fomu kimya kimya na kuondoka.