Asalam aleykum na Bwana Yesu
Asifiwe.
1.0. Awali ya yote ninaomba kuchukua nafasi hii
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kukutana nanyi siku hii ya leo.
Napenda pia kuwashukuru kwa moyo mmoja kwa kuitikia wito wangu wa kuja kwenye
mkutano huu muhimu kwetu sote.
2.0. Ndugu zangu; mwaka huu wa 2015 ni mwaka muhimu
kwetu sote Wa-Tanzania kwa sababu kwa mara ingine tena tunapata nafasi pekee ya
kuchagua viongozi wetu watakaotuongoza katika kipindi cha miaka 5 katika ngazi
mbali-mbali. Uchaguzi mkuu ulioko mbele yetu utahusu kumchagua Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Rais wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Wabunge,wawakilishi,masheha na Madiwani.
3.0. Ndugu Wanahabari; Kupitia kwenu mkutano wetu
wa leo ni kwa ajili ya KUWATANGAZIA RASMI kwamba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu
nitagombea nafasi ya UBUNGE JIMBO LA ARUSHA KUPITIA TIKETI YA CHAMA CHA
MAPINDUZI. Iwapo wana CCM na Chama changu kita ridhia.Nia hii nimeshawarifu
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi – Wilaya ya Arusha. Leo hii sasa ninasema rasmi
kwa WAKAZI NA WANANCHI WA WILAYA YA ARUSHA kwamba wakati ukifika nitaenda ofisi
ya CCM – Wilaya na kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo ya UBUNGE KWA MWAKA
2015.
4.0. Mimi kwa jina naitwa MUSTAFA ABDULLA PANJU ni
mwanachama hai wa Chama Cha Mapinduzi kwa kadi namba 1608369. Mimi pia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Utalii ya BUSHBUCK SAFARIS.
5.0. Kwa nafasi hii ya leo sitapenda kueleza
matarajio yangu na ya Chama kwa Wananchi Wa Wilaya ya Arusha kwa sababu Chama
bado hakijatoa ILANI YAKE YA UCHAGUZI 2015. Itakapotolewa nitaweza kueleza
niliyonayo kwa maendeleo yetu ya Wilaya ya Arusha.
6.0. Kwa sasa naomba tu niseme yafuatayo muhimu
sana:-
a) Ninaomba kuwashauri Wananchi na Wagombea
Wenzangu kwamba KUGOMBEA SIYO KUGOMBANA. Maana imezoeleka sana na ni hatari
kwamba Wagombea mara nyingi hujizolea sifa au umaarufu kwa kuwapaka upande
mwingine matope, kashfa na sifa mbaya ambazo baada ya uchaguzi hugundulika siyo
za kweli. Wakati huo kiongozi asiyefaa huwa ameshachaguliwa na hatasaidia
Wananchi kwa kipindi cha miaka 5. Kiongozi mzuri anaachwa pembeni.
b) Kwa hivyo Wagombea wote wa nafasi ya Ubunge katika
Chama lazima kujenga UNDUGU,UPENDO na URAFIKI wakati wote ili kuepuka kujenga
makundi ndani ya Chama kwa misingi mbali-mbali ya UKABILA, UDINI na hata RANGI.
Sisi sote ni WATANZANIA wenye nia ya kuwatumikia Wananchi kwa maendeleo ya
Wilaya,Mkoa na Taifa kwa ujumla.
c) Mimi binafsi – MUSTAFA ABDULLA PANJU katika
harakati hizi zinazokuja za kampeni na Uchaguzi ndani ya Chama na hata baadaye
na Wenzetu wa Vyama Vingine vya Siasa sitamsema mtu binafsi au watu kwa mambo
yao. ILA NITAZUNGUMZA MTAZAMO WANGU KWA MISINGI YA KIONGOZI TUNAYEMTAKA KWA
KUWAONGOZA WANANCHI KWA MAENDELEO YETU WOTE.
ILANI YETU YA CHAMA 2015 ITAKUWA DIRA KATIKA
KAMPENI YANGU.
7.0 Suala hili la makundi na vikundi iwe katika
Chama la kwa Wananchi wote kwa ujumla tuliangalie kwa umakini ni kuliacha
kabisa kwa sababu linajenga UHASAMA ndani ya Chama na pia uhasama unaoleta
ubaguzi ndani ya nchi kwa ujumla. Tuombe Mwenyezi Mungu tuwe na uchaguzi wa
AMANI NA UPENDO ndani ya Chama na pia wakati wa Uchaguzi Mkuu.
8.0 Ndugu zangu kwa nafasi hii naomba
kurudia tena kutangaza nia yangu kwamba itakapofika wakati nitaenda kuchukua
fomu kwenye ofisi yetu ya Chama Cha Mapinduzi – Wilaya.
Kwa nafasi hii nataka nitoe wito kwa Wananchi wa
Arusha na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi. Ili tuweze kushinda kila mmoja
aende akajiandikishe kwenye vituo vilivyoainishwa hapa wilayani.
Wakati ndio huu.
9.0 Baada ya hapo nitatekeleza yatakayofuatia kwa
kuzingatia KANUNI NA SHERIA ZILIZOWEKWA NA CHAMA CHETU – KATIKA KUENDESHA
KAMPENI.
10. Naomba tena kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa
kuja kunisikiliza.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU TUBARIKI WATANZANIA
WOTE
Ahsante Sana
Mustafa Abdulla Panju