KINYANG'ANYIRO cha kuwania Ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini jana kilianza
kwa mbwembwe baada ya wanachama watano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza
kuwania ubunge katika Jimbo hilo.
Wanasheria wawili wa kujitegemea wa Jijini Arusha, Edmund Ngemela na Victor
Njau ndio waliofungua pazia la kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kwa wana CCM wa
Arusha Mjini kutaka kuteuliwa kuwania kiti hicho.
Njau ndiye mwana CCM aliyekwenda kuchukua fomu akiwa na msururu wa wapambe
wa chama hicho, huku wakiimba nyimbo nyingi za kuwataka wanachama wa CCM
kumuunga mkono mgombea huyo, ambaye wanadai ana sifa zote za kulikomboa jimbo
hilo ambalo liko Chadema.
Wengine waliochukua fomu lakini hawakuwa na shangwe na mbwembwe nyingi ni
Mahamudu Omari, Mosses Mwizarubi na Swalehe Kiluvia, ambao waliingia kuchukua
fomu kimya kimya na kuondoka.